Friday, January 3, 2020

UTUNGAJI WA KAZI ZA FASIHI ANDISHI
Utungaji wa kazi za fasihi andishi nii mada inayogusa au inayohusu ubunifu wa maandishi.
Kubuni ni kutnga kisa kutokana na matukio ambayo mwandishi ana uzoefu nayo kupitia milango yake ya ufahamu.
Uwezo wa msanii kueleza visa vya uongo kutokana na matukio ya kweli kwa lengo la kuburudisha, kuelimisha, au kuakisi hali halisi ya jamii hiyo ni kutunga.
Kimsingi siku zote msanii hatungi kitu ambacho hakipo duniani bali hutunga kutokana na mambo yaliyomo ndani ya jamii husika.
                                         Utungaji wa hadithi
Hadithi:ni ni kazi ya sanaa ya sanaa inayotumia lugha ya nathari. Hadithi yaweza kuwa ni masimulizi ya kweli au ya kubuni .Sanaa ya hadithi ni kazi ya mtu yenye wigo wa uyakinifu ambao unafungamana na wakati na mazingira.
Kwa kawaida masimulizi yanayokuwa katika hadithi yanaweza kumhusu mtu mmoja au watu wengi piamasimulizi hayo yanaweza kuhusu mambo yaliyotokea au yanayoweza kutokea. Hadithi hutofautiana kwa sababu ya tofauti za uwezo wa wasanii wa hadithi yenyewe.Kwa hiyo uwezo wa msanii ni muhimu katika ujenzi wa  hadithi na pia sio tu uwezo wa msanii aidha wakati mwengine na lengo la msanii mwenyewe.
                                            Tanzu za hadithi
Kuna aina mbili za hadithi .Ambazo ni
Hadithi fupi (visa)
Hadithi ndefu (riwaya)
Hadithi fupi:Ni aina ya kazi ya sanaa ya utanzu wa hadithi inayotumia lugha iliyoandikwa katika nathari au iliyo katika masimulizi kama haijaandikwa.
Hadithi fupi huwa na tukio moja au mawili na mawanda yake sio mapana sana,haina mchangamano mkubwa na matukio.Wahusika wa hadithi fupi ni wachache ukilinganisha na hadithi ndefu na hutendeka kwa muda mfupi.
            Mambo muhimu ya kuzingatia katika utunzi wa hadithi
Maudhui:mwandishi ana uhuru wa kuandika kitu chochote ambacho kina manufaa kwa jamii na umma kwa ujumla pia maudhui ya hadithi hutofautiana toka jamii moja na nyingine na hutofautiana na mazingira na mahitaji ya jamii hiyo.hadithi hujengwa na dhamira kuu na dhamira ndogo ndogo
Muundo wa hadithi:Muundo ni mpangilio wa visa na matukio katika kazi ya fasihi andishi.Mtunzi mzuri ni Yule anaejua kupangilia visa na matukio na kusuka visa vyake kwa umakini zaidi kiasi cha kumvutia msomaji wake awe na shauku ya kuendelea kusoma kazi hiyo ya fasihi. Mara nyingi hadithi huwa na muundo wa msago, riwaya huwa na muundo wa rukia na msago.
Mtindo wa kazi:Kazi iliyo nzuri mara nyinmgi huwa na vionjo kwa msomaji, msanii inabidi atumie mbinu mbali mbali za kumvutia msomaji kwani msanii anaweza kutumia mbinu za fasihi simulizi pia anaweza kuchanganya tanzu za fasihi katika tanzu yake hiyo.Pia monolojia na dayalojia.
Matumizi ya lugha:Lugha ndio nyenzo kuu ya kazi yoyote ya fasihi,kwani kwa kiasi kikubwa lugha husaidia katika kuunda fani na maudhui ya kazi ya fasihi.Ni vyema mtunzi akitumia lugha yenye vionjo ili kuweza kuwa na umakini kwa msomaji .halikadhalika msanii inabidi atumie usanii katika kuweza kumpa kila mhusika na lugha yake ili imsaidie katika kutambulisha mhusika wa kazi hiyo pia lugha yake iwe inaendana na wasifu wa mhusika wa kazi hiyo.Vilevile lugha iwe na tamathali za semi kama vile sitiari,tafsida,tanakali sauti,tashbiha,tashhisi lugha ya taswira na mbinu nyengine za kisanaa
Uteuzi na uumbaji wa wahusika:Mwandishi anapswa kuchagua na kuumba wahusika wake kiasi cha kukubalika na hali halisi kitabia na maumbile.Mfano kama mhusika ni kiongozi basi aonekane ni kiongozi kweli.Riwaya huwa na wahusika wakuu na wahusika wasaidizi wote hujengwa na kuelezwa kiurefu.
Uteuzi wa jina la kitabu(Hadithi):Msanii anapaswa kuwa makini katika kubuni jina la kitabu kwa sababu jina ndilo linalomvutia msomaji ,vilevile msanii anapaswa kuzingatia katika kubuni jina hilo kwani jina la kitabu linapawa liendane na maudhui yaliyomo ndani ya hadithi hiyo.
Uteuzi wa mandhari:Mandhari ni sehemu au mahali ambamo kazi ya fasihi inafanyika.Ujenzi mbaya wa mandhari huleta athari mbalimbali katika hadithi na riwaya.Kuna mandhari za aina mbili ambazo ni mandhari ya kubuni na mandhari halisi. Vilevile mandhari yakielezwa vizuri huimarisha mfumo wa hadithi/riwaya pamoja na ujengaji wa wahusika wake.Mandhari ikiibuliwa vibaya huathiri mfumo mzima wa kazi ya fasihi ,pia matumizi ya vifaa viendane na wakati.
Riwaya:Ni kisa changamano ambacho huweza kuchambuliwa na kupimwa kwa mapana na marefu kifani na kimaudhui. Au Riwaya ni masimulizi marefu ya kubuni yaliyoandikwa ambayo hujumuisha wahusika wengi mawanda mapana ya kimandhari pamoja na kuelezea tukio zaidi ya moja.
Riwaya hufungamana na wakati  yaani visa vinaendana/vinatendeka katika wakati Fulani,ina mawanda mapana kwa upande wa yale yanayozungumzwa wakati na mahali pia matukio hayo, vile vile riwaya ina sifa ya uchangamano wa wa visa,dhamira,tabia na wahusika.
                 Tofauti kati ya hadithi fupi na riwaya
Zipo tofauti mbalimbali zinazojitokeza kati ya utanzu wa hadithi fupi na utanzu wa riwaya.Miongoni mwa tofauti hizo ni kama zifuatazo:
Tofauti ya upana wa  mawanda:riwaya hutumia mawanda mapana kwani kila jambo hupewa uzito wake na kuelezwa kwa mapana ya kutosha lakini hadithi fupi mambo yake huelezwa kwa ufupi na mkato tu.
Tofauti ya wahusika:Riwaya hutumia wahusika wengi na wahusika hao huelezwa kiurefu,riwaya pia huhusisha mhusika mkuu na wahusika wasaidizi lakini hadithi fupi huwa na wahusika ambao huwa hawaelezwi kwa urefu ukilinganisha na wahusika wa riwaya.
Tofauti ya urefu:Riwaya ni kazi yakubuni ambayo ni ndefu urefu wake unatokana na uchangamano wa visa na wahusika wengi lakini hadithi fupi ni kazi ya sanaa ambayo ni fupi kiasi kwamba inaweza kusomwa kwa kikao kimoja na kumaliza.
Tofauti ya uchangamano:Riwaya ina muundo changamano kutokana na wingi wa matukio lakini hadithi fupi ina muundo sahili usiochangamana kwani hadithi fupi hueleza juu ya tukio moja tu.
Tofauti ya dhamira:kikawaida riwaya huwa na dhamira kuu na dhamira ndogondogo lakini hadithi fupi huwa na dhamira chache wakati mwingine huwa na dhamira moja tu.
                                    Utunzi wa Tamthiliya
Tamthiliya ni utungo wa kidrama ambao ni aina mojawapo ya maandishi ya sanaa za maonyesho.Au Tamthiliya ni mchezo wa kuigiza unaoigizwa jukwaani.Ni sanaa inyoonyeshwa kwa ufundi,Tamthiliya huonyesha matendo ya wanajamii kwa njia ya kuigiza,maigizo ambayo hatimaye huweza kuonyeshwa kwenye majukwaa kwenye sanaa za maonyesho.
                                     Sifa za Tamthiliya
Tamthiliya huwa na sifa za kawaida za sanaa za maonyesho miongonimwa sifa hizo ni kama:
Dhana inayotendeka
Mtendaji
Uwanja wa kutendea
Watazamaji(Hadhira)
Kusudio la kisanaa:Hii hutupa uhakika kuwa kinachotendeka hapo kimedhamiriwa kwa sanaa na sio kitu kingine
Muktadha wa kisanaa:Unafafanua mazingira ya tukio hilo
Ubunifu:Ni muhimu ili kutofautisha kati ya tendo la dhati na tendo la kisanaa.
                          Dhima za Tamthiliya 
Tamthiliya ina dhima mbalimbali kwa jamii baadhi ya dhima hizo ni kama :
Kuelimisha jamii
Kutunza kumbukumbu (mali)za jamii
Kuonya na kuadabisha jamii
Kuhamasisha shughuli za kimaendeleo
Kuburudisha jamii
                  Vipengele/Muundo wa Tamthiliya
Hadithi(Simulizi):Huwa ni kisa cha kubuni au cha kweli au mchanganyiko wa vyote viwili,hadithi huwa na mzozo Fulani wa pande mbili hadi kufikia mwisho wake. AB- chanzo au mwanzo wa mchezo, chanzo cha mgogoro huelezwa na tamthiliya kama ni hali ya majonzi au furaha, wakati na mahali panapotokea vitendo vya hadithi wahusika hutambulishwa. BC- kukua kwa mgogoro,mvutano baina ya pande mbili  hujitokeza chanzo cha mgogoro huelezwa, njia za kutatua tatizo na kujaribu kutatua tatizo hilo. C- tatizo limefika kileleni ambapo uwezekano wa kulitatua huwa haupo. CD- mgogoro huanza kuleta mshtuko na taharuki hutokea. DE- mgogoro hufika mwisho.
Vitendo:Tamthiliya hugawanyika katika sehemu kuu ziitwazo vitendo. Kila kitendo huzingatia tendo moja kuu,tamthiliya huwa na vitendo vitano,vitendo hugawanyika katika sehemu ndogondogo ambazo ni maonyesho ambapo onyesho moja huwa na tukio moja linalotendeka mahala pamoja, onyesho moja hutenganishwa na onyesho jengine kutegemea na kitu kinachosimuliwa, kumalizika kwa tukio huashiria wahusika kuondoka, kuzima taa nakadhalika.
Wahusika:Ni viumbe hai wanaobebeshwa matendo ya mwanadamu katika kazi ya fasihi, uhusika wao huhusiana na kile wanachokizungumzia, na pia wahusika wake hawatofautiani na wahusika wa hadithi wa hadithi ambapo kuna wahusika wakuu na wahusika wadogo.
Dayalojia:Ni Mazungumzo/majibizano baina ya wahusika .Kufanikiwa kwa msanii kutategemea ni jinsi gani anatunga dayalojia yake kwa namna ya kuvutia na azingatie maneno machache yanayojitosheleza, pia monolojia huwerza kutumika pale ambapo mhusika anakuwa anawaza mwenyewe moyoni.
Mbinu nyengine:Pia msanii wa tamthiliya anaweza kutumia mbinu mbalimbali ili kuipamba na kuifanya tamthiliya yake ivutie kwa hadhira na hatimaye kuweza kuibua dhamira lengwa kwa jamii,baadhi ya mbinu hizo ni kama matumizi ya mbinu ya utambaji,ngano nakadhalika.

No comments:

Post a Comment

UTUNGAJI WA KAZI ZA FASIHI ANDISHI Utungaji wa kazi za fasihi andishi nii mada inayogusa au inayohusu ubunifu wa maandishi. Kubuni ni kutn...